SERIKALI YASISITIZA KINGA NA UCHUNGUZI WA MAPEMA KATIKA MATIBABU YA MOYO.

SASA TAKWIMU YA WANANCHI WALIYOJITOKEZA KUPIMA YAZIDI 1000 NA BADO WANAZIDI KUMIMINIKA ALMC JIJINI ARUSHA.

Na Lucas Myovela - Arusha.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha na maeneo ya jirani kuzingatia afya zao kwa kufanya uchunguzi wa mara kwa mara, huku akisisitiza umuhimu wa kujiunga na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote kama nguzo muhimu ya kufanikisha azma ya afya bora kwa kila Mtanzania.

Akizungumza wakati wa ziara yake katika Kambi Maalum ya Uchunguzi na Matibabu ya Magonjwa ya Moyo inayofanyika katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) Januari 4, 2026, Mkude alisema kuwa magonjwa yasiyoambukiza yameendelea kuwa tishio kubwa kwa afya ya jamii, hususan magonjwa ya moyo, shinikizo la damu na kisukari.


Pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuimarisha sekta ya afya kupitia programu ya Tiba Mkoba, inayosogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi kwa kupatiwa matibabu ya kibingwa.


“Kupitia programu hii, Watanzania wengi wamepata fursa ya kupata huduma za kibingwa na kibingwa bobezi bila kusafiri umbali mrefu, jambo ambalo limepunguza gharama na kuokoa maisha,” alisema Mkude.


Aidha, alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter R. Kisenge, kwa kuamua kuleta huduma hizo katika Mkoa wa Arusha, hususan Wilaya ya Arusha Mjini, akibainisha kuwa mkoa huo ni kitovu cha utalii na unahitaji huduma bora za afya kwa wananchi na wageni.


Akizungumza kuhusu ukubwa wa tatizo la magonjwa ya moyo, Mkude alinukuu takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinazoonesha kuwa zaidi ya vifo milioni 17.5 duniani, sawa na asilimia 32 ya vifo vyote, husababishwa na magonjwa ya moyo. Aliongeza kuwa takwimu za kitaifa zinaonesha Mkoa wa Arusha kuwa miongoni mwa maeneo yenye idadi kubwa ya wagonjwa wa magonjwa yasiyoambukiza.


Katika kuimarisha mapambano hayo, Mkuu wa Wilaya aliwahimiza wananchi kujiunga na bima ya afya mapema ili kujikinga na mshtuko wa kifedha unaoweza kujitokeza wakati wa matibabu ya muda mrefu au ya kibingwa.

“Bima ya afya inalinda familia, inaleta utulivu wa kifedha na kuhakikisha matibabu yanapatikana kwa wakati,” alisisitiza.


Mkude alieleza kuwa Wilaya ya Arusha tayari imezindua mpango wa mafunzo ya uhamasishaji kuhusu afya katika ngazi za wilaya, kata na mitaa, ili kuongeza uelewa wa jamii kuhusu kinga na tiba za magonjwa yasiyoambukiza.


Akitoa taarifa ya mafanikio ya kambi hiyo, alisema kuwa tangu kuanza kwake tarehe 29 Desemba 2025 hadi 4 Januari 2026, wananchi zaidi ya 1000 wamehudumiwa, wakiwemo watu wazima zaidi ya 700 na watoto 100, sawa na wastani wa wagonjwa 155 hadi 200 kwa siku.


Aliongeza kuwa vipimo vya kibingwa ikiwemo ECHO na ECG vimefanyika, huku wagonjwa 53 wakitathminiwa kwa ajili ya upasuaji wa moyo. Kati yao, upasuaji mkubwa tano tayari umefanyika, na wagonjwa 45 wamepatiwa rufaa kwenda JKCI Dar es Salaam, wakiwemo watu wazima 37 na watoto 8.


Kwa kuwa kambi hiyo itaendelea hadi tarehe 9 Januari 2026, Mkuu wa Wilaya alitoa wito kwa waandishi wa habari kuhakikisha taarifa hizo zinawafikia wananchi wengi zaidi ili wajitokeze kunufaika na huduma hizo muhimu.

Kwa mujibu wa tathmini ya awali, kambi hiyo imefanikiwa kubaini wagonjwa wanaohitaji ushauri, tiba na upasuaji wa moyo kwa watu wazima na watoto, pamoja na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu huduma za JKCI na ALMC, hali inayoweka msingi wa uwepo wa huduma hizo kwa kipindi cha miaka 20 ijayo.


Mkude alisema muunganiko wa JKCI na ALMC ni wa kimkakati, hasa ikizingatiwa kuwa Arusha inajiandaa kuwa miongoni mwa wenyeji wa mashindano ya AFCON, sambamba na ajenda ya kitaifa ya kukuza Utalii wa Tiba (Medical Tourism).


Akihitimisha, aliwapongeza na kuwashukuru wataalamu wote wa afya kwa kujitoa kwao bila kuchoka, akisisitiza kuwa Serikali ya Mkoa wa Arusha inatambua na kuthamini mchango wao katika kuimarisha afya za Watanzania.












Comments