Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Kairuki alisema kuwa elimu kwa umma ni nguzo muhimu katika utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, akibainisha kuwa uelewa mdogo wa sheria hiyo unaweza kusababisha ukiukwaji wa faragha na haki za wananchi.
“Maafisa wa ulinzi wa taarifa binafsi mliohitimu leo mna wajibu wa kisheria kuhakikisha elimu hii inatolewa ndani ya taasisi zenu. Serikali haitakubali visingizio vya kutokujua sheria, uzembe au ucheleweshaji wa utekelezaji,” alisema Waziri Kairuki.
Aidha, Waziri huyo alisisitiza kuwa elimu ya ulinzi wa taarifa binafsi inapaswa kutekelezwa kitaifa kwa ushirikiano kati ya taasisi za umma na binafsi pamoja na sekta mbalimbali ikiwemo fedha, mawasiliano, afya, elimu, vyombo vya habari, asasi za kiraia na makundi yote yanayohusika na ukusanyaji au uchakataji wa taarifa binafsi.
Aliongeza kuwa kila Afisa wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi ana wajibu wa kuhakikisha taasisi yake inazingatia kanuni za msingi za ulinzi wa taarifa ikiwemo uhalali, uwazi, matumizi ya taarifa kwa madhumuni maalum, usalama wa taarifa na heshima ya faragha ya wananchi.
Bw. Adadi alionya kuwa kutotekeleza Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ni sawa na kuhatarisha faragha, usalama na haki za msingi za wananchi.
“Kukosekana kwa ulinzi wa taarifa binafsi kunadhoofisha imani ya wananchi na kuathiri maendeleo ya uchumi wa kidijitali,” alisema.
Akieleza lengo la mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Dkt. Emmanuel Mkilia, alisema kuwa mafunzo yalilenga kuwaandaa Maafisa wa Rasilimali Watu na Maafisa wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi wenye uwezo wa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria ndani ya taasisi zao.
Dkt. Mkilia alisisitiza kuwa lengo kuu ni kuhakikisha ukusanyaji, uchakataji, uhifadhi na matumizi ya taarifa binafsi yanafanyika kwa kuzingatia matakwa ya sheria, kanuni na viwango vya kitaaluma vinavyolinda haki ya faragha ya wananchi.
Kwa mujibu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, jumla ya taasisi 178 zilishiriki mafunzo hayo, zikiwemo taasisi 28 za serikali, taasisi 38 kutoka sekta ya utalii na taasisi 112 kutoka sekta nyingine mbalimbali zinazojihusisha na ukusanyaji na uchakataji wa taarifa binafsi.




Comments
Post a Comment