VETA NGUZO MUHIMU YA KUANDAA VIJANA NGUVU KAZI KATIKA UJUZI WA KISEKTA.

🔺️MABADILIKO YA SERA YA ELIMU NA MAFUNZO YATIA MSISITIZO KATIKA ELIMU YA UFUNDI KUANZIA MSINGI.

Na Lucas Myovela - Arusha.

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesema VETA ni nguzo muhimu katika kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi kwa sekta za ukarimu na utalii, ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika pato la taifa. 

Akizungumza Januari 05, 2026 alipokagua uendeshaji Mafunzo ya Amali yanavyotolewa katika Chuo cha VETA cha Mafunzo ya Hoteli na Utalii Njiro Arusha Mhe. Ameir amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, zinazosisitiza elimu ya ujuzi na maandalizi ya jamii iliyoelimika na yenye ushindani wa kimataifa.  


Naibu Waziri amesema chuo hicho kimekuwa mfano wa kuigwa kwa kutoa mafunzo ya ukarimu na utalii kwa ubora yanayozingatia kutoa ujuzi wa vitendo.


Chuo hicho pia kinaendesha hoteli ya mafunzo kwa ajili ya wanafunzi inayowezesha kuongeza mapato ya ndani na kupunguza utegemezi wa bajeti ya Serikali.  

Aidha, Naibu Waziri huyo amebainisha kuwa maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo yameweka msisitizo mkubwa kwenye elimu ya ujuzi kuanzia ngazi ya msingi. Ameelekeza VETA kupanua wigo wa kuandaa wakufunzi na walimu tarajali wa mafunzo ya amali, hususan katika ukarimu na utalii, ili kukidhi mahitaji ya shule za sekondari na vyuo vya ufundi. 


Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kutoa rasilimali na vifaa vya kisasa, pamoja na kuajiri wakufunzi wenye mbinu bora za ufundishaji huku akiitaka VETA kuendeleza ushirikiano na wadau wa sekta binafsi ya ukarimu na utalii ili kuongeza ajira na mchango wa sekta hiyo katika pato la taifa.


Mhe. Ameir amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya utoaji wa mafunzo ya ufundi na ufundi stadi, ili kufanikisha azma ya Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA, Anthony Kasole amesema taasisi hiyo inaendelea kuhakikisha vijana wanapata ujuzi unao endana na mahitaji ya soko la ajira ndani na nje ya nchi.


CPA, Kasole, ameongeza kuwa katika kuhakikisha dira ya taifa 2050 VETA haijawaacha vijana wote katika fani mbalimbali ili kuhakikisha wanapata ujuzi kwa ustawi wa taifa na ukuaji wa uchumi.







Comments