🔻HUU NI MPANGO MAALUMU WA KUTEKELEZEZA SERA YA ELIMU NA MAFUNZO KUFIKIA DIRA YA TAIFA 205O.
Na Lucas Myovela - Arusha.
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatekeleza mpango maalumu wa kujenga uwezo wa nchi katika teknolojia za Takwimu, Akili Unde na Sayansi Shirikishi (DS/AI+) kupitia Programu ya Samia Scholarship Extended ambapo vijana 50 wanajiandaa kupelekwa nje ya nchi kusoma shahada za kwanza katika fani hizo, hatua itakayoongeza ushindani wa Tanzania katika mageuzi ya kidijitali na kuzalisha ajira mpya.
Mpango huu umeelezwa kuwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambazo zimeweka kipaumbele katika kujenga jamii iliyoelimika na yenye ujuzi wa kushindana kimataifa.
Hayo yameelezwa Januari 05, 2026 jijini Arusha na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, alipokutana na viongozi na wanafunzi wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) ambapo amepongeza jitihada za taasisi hiyo katika kuendeleza tafiti na bunifu za kiteknolojia zinazojibu mahitaji ya jamii na viwanda, sambamba na kuandaa vijana kushiriki kikamilifu katika mageuzi ya kidijitali.
Aidha, Naibu Waziri huyo amesisitiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanapata ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira ndani na nje ya nchinkwani NM-AIST ni nguzo muhimu ya kuzalisha wataalamu wa sayansi, teknolojia na ubunifu barani Afrika, sambamba na kuimarisha uwezo wa taifa kushindana kimataifa.
Katika ziara hiyo, Mhe. Ameir alipata fursa ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa hosteli maalumu kwa ajili ya wanafunzi wa kike wenye watoto na mahitaji maalumu. Mradi huo umefikia asilimia 80 ya utekelezaji na umetajwa kuwa ubunifu wa hali ya juu katika kutoa fursa sawa kwa wote, hatua inayounganisha jitihada za Serikali za kumwezesha mtoto wa kike kupata nafasi sawa katika elimu ya juu.
Makamu Mkuu wa Taasisi ya NM-AIST, Prof. Maulilio Kipanyula amesema kuwa mpaka sasa taasisi hiyo imewawezesha vijana kupata udahili katika vyuo mbalimbali duniani ambapo wanafunzi 16 wamepata nafasi nchini Afrika Kusini, 29 wamepata nafasi nchini Ireland, na watano wako katika hatua ya mahojiano ya ana kwa ana Kwa ajili ya kupata udahili
Aidha, Prof. Kipanyula ameongeza kuwa ujenzi wa hosteli maalumu ni utekelezaji wa mkakati wa taasisi kuongeza idadi ya wanafunzi kutoka 600 hadi kufikia 1000, huku wanaoishi katika mabweni wakiongezeka kutoka 279 hadi 779.
Comments
Post a Comment