DKT. MWIGULU AITAKA WIZARA YA ELIMU KUONGEZA WANAFUNZI KUPITIA SAMIA SCHOLARSHIP KUPATA NAFASI MASOMO ELIMU YA JUU.

🔺️AZINDUA MABWENI YENYE THAMANI YA BILIONI 9.07 KATIKA TAASISI YA SAYANSI NA TEKNOLOJIA YA NELSON MANDELA.

Na Lucas Myovela - Arusha.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuongeza vyanzo vya uhakika vya kufadhili wanufaika wa Samia Scholarship ili kuongeza idadi ya wanafunzi wanaopata nafasi za masomo ya Elimu ya juu.


Pia Dkt. Mwigulu ameitaka Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela kuhakikisha wanafunzi wanao hitimu hapo wawe na uwezo bunifu wa kujiajili na kuajili wengine katika uwanda wa kitaifa na kimataifa.


Dkt. Nchemba ameyasema hayo Februari 22, 2026 katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wakike wenye familia pamoja na wanafunzi wenye mahitaji maaluum katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela iliyopo Nambala Wilaya ya Meru Mkoani Arusha.


Dkt. Mwigulu, ameeleza kuwa Serikali imedhamilia kuongeza wigo wa vyuo vikuu hapa nchini ilikugikia mafanikio ya Dira ya Taifa 2050 kwa lengo la kuandaa watanzania wenye ushindani katika Sayansi ma Bunifu.

"Chuo kinatakiwa kuwa bunifu hasa kulenga katika kutatua changamoto za wananchi moja kwa moja, Mradi huu ni lengo la kuendeleza elimu ya juu katika nyanja ya Sayansi, Teknolojia na Bunifu, Serikali imeongeza jitihada katika kukuza sekta ya elimu, mfano hapa nimeona unaweza kukausha tumbaku ukiwa umevaa suti, hizi ndizo bunifu tunataka na nyingine nyingi". Amesema Mwigulu.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa mchakato wa uteuzi wa wanafunzi katika utoaji wa udadhili wa Samia Skolashipu ambao ni mpango wa kukuza vipaji vya sayansi na teknolojia unafanywa kwa uwazi na kuzingatia sifa stahiki zilizowekwa.


Prof. Mkenda amesisitiza kuwa kamati maalum huru inasimamia hatua zote ili kuhakikisha haki inatendeka na kuzuia upendeleo na kwamba kuna kipindi cha tathmini ya wiki sita kinachotumika kufuatilia wanafunzi hao, ili kuhakikisha wanaendelea vizuri na kuepuka matumizi mabaya ya fursa walizopewa.


Amefafanua kuwa lengo ni kutoa fursa kwa watoto wa wakulima na wafugaji kupata elimu bora na nafasi katika sekta ya teknolojia, ili kuimarisha usawa na maendeleo ya taifa.


Prof. Mkenda ameeleza kuwa mpango huo unatoa nafasi kwa wanafunzi wenye uwezo mkubwa kushiriki masomo na mafunzo ya vitendo katika nyanja za teknolojia ya habari, hususan Sayansi ya Data, Akili Bandia (Al), na Sayansi za DLR (Deep Learning na Robotics).


Prof. Mkenda ameongeza kuwa Programu ya Samia Scholarship Extended inawapeleka Wanafunzi katika Vyuo mahiri ambavyo vinasaidia wanafunzi kupata nafasi za kujifunza na kushiriki katika mafunzo ya vitendo kwenye makampuni, ili kukuza umahiri na kuandaa kizazi kipya cha wataalamu wa teknolojia barani Afrika.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof, Daniel Mushi, amesema kuwa uwepo wa Taasisi hiyo nchini unaipa heshima nchi katika kuendeleza elimu ya juu yenye mwelekeo wa kimataifa.


"Taasisı ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) ni moja ya taasisi tatu pekee barani Afrika zilizoundwa mahsusi kwa lengo la ukujenga uwezo wa bara kujitegemea katika kuzalisha teknolojia zinazokidhi mahitaji halisi ya jamii kupitia utafiti, ubunifu na mafunzo ya ngazi ya umahiri na uzamivu". Amesema Prof. Mushi


"Kwa sasa, wanafunzi wa kigeni wanaunda takribani asilimia tisa ya jumla ya wanafunzi wa taasisi hii, jambo linaloonyesha mchango wake katika kuunganisha Afrika kupitia maarifa na teknolojia". Amesisitiza Prof. Mushi.

Awali Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Prof. Maulilio Kipanyula, ameeleza kuwa mradi wa hosteli za wanafunzi umebuniwa kwa lengo la kuongeza fursa za masomo katika Maeneo ua Sayansi na Teknolojia kwa wanawake.


Prof. Kipanyula, amesema kuwa jengo hilo limebuniwa likiwa na mfumo wa mabawa matano na lina jumla ya vyumba 174, ambapo vyumba 160 ni vya kawaida na vinajitegemea (self-contained) kwa wanafunzi wa shahada za uzamili na uzamivu, huku vyumba 20 vikiwa maalum kwa wanafunzi wenye watoto wadogo na wanafunzi wenye mahitaji maalum.


"Hiinalenga kutoa mazingira salama na jumuishi yanayowawezesha wanafunzi wote kusoma bila vikwazo na jengo hilo litaanza kwa kuhudumia wanafunzi 80 na lengo ni kufikia uwezo wa kuchukua wanafunzi 150". Amesema Prof. Kipanyula.


Aidha, ameeleza kuwa jumla ya gharama ya mradi ni shilingi bilioni 9.07, ambapo serikali tayari imetoa zaidi ya shilingi bilioni 6 huku akisisitiza kuwa uwekezaji huo ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya kuendeleza elimu ya juu na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha utafiti na ubunifu barani Afrika.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Michezo na Utamaduni, Mhe. Husna Sekiboko, amesema kuwa hosteli inayojengwa katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela ni hatua muhimu ya kuimarisha mazingira ya kujiífunza na kupunguza changamoto za malazi kwa wanafunzi.


Mhe. Sekiboko ameeleza kuwa hosteli mpya itasaidia wanafunzi wa kike, hususan wanaosoma masomo ya sayansi na Teknolojia katika ngazi za shahada za Umahiri na Uzamivu kwa kuwapa nafasi ya kuishi katika mazingira tulivu kielimu.

"Hosteli hii itawawezesha wanafunzi wenye watoto kuishi nao, jambo litakalowaondolea mzigo wa kutafuta mahali pa kuwaacha watoto na hivyo kuimarisha usawa wa kijinsia katika elimu ya juu, hii ni tafsiri halisi ya kazi na utu". Amesema Mhe. Sekiboko.


Aidha Mhe, Sekiboko amesisitiza kuwa utekelezaji bora wa mradi huo ni matokeo ya mshikamano kati ya serikali, wizara husika na wadau mbalimbali, na kutoa wito kwa serikali kuendeleza ushirikiano ili kutatua changamoto nyingine za sekta mbalimbali, ambapo ameahidi kuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Michezo na Utamaduni itahakikisha mipango yote mizuri inakamilika kwa manufaa ya wananchi.











Comments