🔺️SERIKALI YA TANZANIA KUPITIA WIZARA YA AFYA YATANGAZA KWA WANANCHI.
Na Lucas Myovela.Wizara ya Afya Nchini Tanzania imetoa tahadhari juu ya uwepo wa mafua makali ya Influeza pamoja na UVIKO-19 ( COVID 19) na kuwataka Wananchi kuchukua tahadhari kubwa.
Taarifa ya Wizara hiyo imesema kutokana na takwimu za ufuatiliaji zilizofanyika kwa kipindi cha mwezi Novemba hadi Aprili ongezeko kubwa la mafua makali ya INFLUEZA na UVIKO-19 hutokea hapa Nchini na Duniani.
Wizara imewataka Watanzania kuchukua tahadhari zifuatazo
— kufunika pua na mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya.
— kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono ili kuepuka misongamano isiyo ya lazima.
— Kuvaa barakoa unapokuwa na dalili, unapokuwa karibu na mtu mwenye dalili au ukiwa kwenye maeneo yenye msongamano
— Kuzingatia usafi binafsi na wa mazingira
— Kuwahi katika kituo cha kutolea huduma za afya kupata matibabu stahiki
— kuepuka kujitibu au kutumia Antibiotiki bila ushauri wa Watalaam wa afya.
Aidha Wizara ya Afya imeeleza magonjwa hayo huambukizwa na kuenezwa kupitia majimaji kutoka kwenye mfumo wa njia ya hewa wa Mgonjwa mwenye maambukizi na husambaa wakati wa kukohoa, kupiga chafya au kuzungumza.
Imeongeza kuwa mafua makali ya Influenza na UVIKO-19 huweza kuenezwa kwa kugusa mazingira yaliyochafuliwa na majimaji yanayotoka kwa mgonjwa ambapo dalili za magonjwa haya ni homa kali, kikohozi, maumivu ya kichwa na mwili, mafua, kuwashwa koo na uchovu.
SERIKALI YAAGIZA KUONGEZA KASI UFUATILIAJI MAGONJWA YA MFUMO WA NJIA YA HEWA.
Serikali kupitia Wizara ya Afya
imeziagiza Hospitali za Rufaa za Mikoa, Taifa, Wilaya na Vituo vya Afya kuongeza kasi ya ufuatiliaji wa magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa pamoja na magonjwa mengine ya mlipuko.
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe ametoa maagizo hayo leo Februari 25, 2026 mkoani Morogoro
wakati akizungumza na Waganga Wakuu Wafawidhi na watendaji wa vituo vya kutoa huduma vinavyofanya ufuatiliaji
wa magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa (Sentinel Surveillance Centers).
"Tunaendelea kuviwezesha vituo vingi zaidi katika ufuatiliaji wa magonjwa ya
mfumo wa njia ya hewa hasa ukusanyaji wa sampuli mapema na kuziwasilisha
mapema maabara ya Taifa, kazi hii ni ulinzj wa nchi dhidi ya magonjwa ya mlipuko na hakuna mbadala", amesema
Dkt. Magembe.
Aidha, Dkt. Magembe ameiasa jamii kuacha matumizi holela ya dawa za "Antibiotiks" ili kudhibiti usugu wa vimelea dhidi ya dawa, jambo linalopelekea wengi kushindwa kupona baada ya kutumia baadhi ya "antibiotiks".
"Mtu akijisikia mafua, kikohozi
vimeambatana na homa, mwili kuchoka kuumwa kichwa nk anakimbilia duka la
dawa kununua antibiotiki, hiyo sio sawa ukihisi unaumwa nenda kwenye kituo cha tiba wakwambie unaumwa nini
baada ya kupimwa badala ya kunywa dawa kiholela" amesema Dkt. Magembe
Katika hatua nyingine, Dkt. Magembe amesema licha ya ugonjwa wa Kipindupindu kuisha, ametoa wito kwa
wananchi kuendelea kuchukua
tahadhari za kujikinga na magonjwa hayo ikiwemo kunawa mikono kwa maji
tiririka na sabuni, matumizi sahihi ya vyoo na kutumia maji safi na salama.
Pia, Dkt. Magembe ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wadau kwa kuendelea
kushirikiana na Serikali katika
kukabiliana na magonjwa ya mlipuko wakiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO), pamoja na Shirika la Kimataifa la PATH.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji wa Magonjwa ya Mlipuko
kutoka Wizara Dkt. Vida Mmbaga amesema, Tanzania imejenga uwezo mkubwa wa kukabiliana na magonjwa ya
mlipuko.
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe akizindua vitabu vya mwongozo wa ufuatiliaji wa magonjwa ya mlipuko na kuvigawa kwa Waganga Wakuu wa Mikoa, Waganga Wafawidhi wa Hospitali za rufaa za Mikoa, Waganga Wakuu Wafawidhi wa vituo vya kutoa huduma vinavyofanya ufatiliaji wa magonjwa wa mfumo wa njia ya hewa kwenye ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika leo Februari 25, 2026 mkoani Morogoro.
Comments
Post a Comment