WAZIRI KIKWETE AWAONYA VIKALI WATUMISHI WA UMMA WALIYO OTA NUNDU MAOFISINI ATAKA MIFUMO YA KIDIGITALI KULINDA TAARIFA ZA UMMA.
SERIKALI YAONYA WATUMISHI WA UMMA MATUMIZI YA MIFUMO ISIYO RASMI,YASISITIZA NIDHAMU YA KIDIGITALI KULINDA USALAMA WA TAARIFA ZA UMMA.
"Nataka niwakumbushe kuwa, kila mmoja aliingia katika Utumishi wa Umma kwa sifa zake, wengine wameingizwa kupitia mitihani ya ajira, wengine kwa nafasi za uteuzi, hivyo kila mmoja akitimiza wajibu wake ni wazi kuwa matokeo mazuri yataonekana". Amesema Ridhiwani Kikwete.
"Kuna baadhi ya Watumishi wa Umma wanatumia barua pepe binafsi kutuma taarifa rasmi za serikali, wanachokifanya ni jambo la hatari sana, tutumie mifumo yetu iliyotengenezwa na wataalam wetu wandani," - Ameongeza Ridhiwani Kikwete
Akisisitiza nidhamu ya kidijitali, Waziri Kikwete alionya matumizi ya barua pepe binafsi kama Gmail, Yahoo na Hotmail katika mawasiliano ya kikazi, akibainisha kuwa mifumo rasmi ya serikali ndiyo yenye viwango vinavyohitajika kulinda nyaraka na taarifa nyeti za umma.
Alisema pia baadhi ya watumishi bado wanatumia njia zisizo rasmi katika miamala na mikopo, jambo linalosababisha hatari za kifedha na kiutumishi licha ya kuwepo kwa mifumo salama ya serikali.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Benedict Ndomba, alisema maazimio ya kikao hicho yatatekelezwa kwa ushirikiano wa wadau wote ili kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ubora wa huduma za umma.
Alieleza kuwa kikao hicho kimejadili kwa kina mada 14 kuhusu utekelezaji wa miradi ya TEHAMA serikalini, kikiweka mkazo katika kuunganisha mifumo ya taasisi za umma kuimarisha ulinzi dhidi ya mashambulizi ya kimtandao, na kuharakisha utoaji wa huduma kupitia majukwaa ya kidijitali.
Katika hafla hiyo, eGA ilikabidhi tuzo kwa taasisi zilizozingatia sheria, kanuni na viwango vya utekelezaji wa miradi ya ТЕНАМА.
Kwa niaba ya Bunge, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Damas Ndumbaro alisema mageuzi ya serikali mtandao yamepunguza gharama za uendeshaji na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Alitolea mfano Bunge kuondoa matumizi ya karatasi na kuhamia mifumo ya kielektroniki, hatua iliyoleta ufanisi mkubwa wa kiutendaji.
Ndumbaro alisisitiza umuhimu wa kuunganisha mifumo ya serikali ili mwananchi apate huduma kwa kutumia namba moja ya utambulisho wa taifa, huku Bunge likiahidi kuendelea kuunga mkono marekebisho ya kisheria na kibajeti yanayohitajika kuharakisha mchakato huo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Toba Nguvilla, alisema kuendelea kwa Arusha kuwa mwenyeji wa mikutano ya Serikali Mtandao ni ishara ya imani ya taifa kwa mchango wa mkoa huo katika mageuzi ya kidijitali.
Alihimiza taasisi za umma kuzingatia kikamilifu sera na viwango vya TEHAMA ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.
Serikali imeagiza waajiri katika taasisi za Umma kuwekeza zaidi katika mafunzo ya wataalamu wa TEHAMA ndani na nje ya nchi, ili kukabiliana na mabadiliko ya haraka ya teknolojia na kuimarisha kinga dhidi ya vitisho vya kimtandao.
Aidha, imehimiza ushirikiano wa karibu kati ya serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo katika kujenga mfumo salama na jumuishi wa huduma za umma.
Katika kuhitimisha, viongozi wa mkutano huo walimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono na uongozi katika kusukuma mageuzi ya kidijitali, wakibainisha kuwa hatua hizo zimeongeza kasi ya utoaji huduma na kuimarisha uwajibikaji serikalini.


















Comments
Post a Comment