WAONGOZA WATALII WAPIGWA MSASA ARUSHA: WAZIRI KIJAJI ASISITIZA UTAALAMU, USALAMA WA WAGENI NA UTALII ENDELEVU

💢TATO NA ZARA TOURS WAKISHIRIKI KIKAMILIFU KUINUA UBORA WA UTALII TANZANIA, WAIPONGEZA SERIKALI KWA KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA WADAU KATIKA MAENDELEO YA SEKTA YA UTALII.Na Lucas Myovela - Arusha.

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, amefungua rasmi mafunzo ya Waongoza Watalii kwa mwaka 2026, akisisitiza umuhimu wa utaalamu usalama na uwajibikaji katika kuimarisha sekta ya utalii nchini.


Akizungumza jijini Arusha Aprili 18, 2026, Dkt. Kijaji alisema waongoza watalii ni nguzo muhimu katika sekta hiyo, kwa kuwa wao ndio wanaokutana na wageni mara tu wanapowasili nchini na kuwa nao kwa muda mrefu zaidi katika safari zao.

"Ni wazi kuwa ninyi ndio mabalozi namba moja wa utalii wetu. Jinsi mnavyowahudumia wageni ndivyo inavyojenga taswira ya Tanzania kimataifa," alisema.


Alibainisha kuwa mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya utalii yanatokana na juhudi za Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa chachu ya kukuza utalii kupitia kampeni mbalimbali zikiwemo filamu za Tanzania (The Royal Tour) na Tanzania ya Kuvutia (Amazing Tanzania).


Kwa mujibu wa Waziri huyo, idadi ya watalii wa kimataifa imeongezeka kwa asilimia 161 kati ya mwaka 2021 hadi 2025 huku mapato ya sekta hiyo yakiongezeka kwa asilimia 238.5 katika kipindi hicho.

"Mafanikio haya yanapaswa kulindwa na kuendelezwa. Ndiyo maana Serikali kwa kushirikiana na wadau kama Chama cha Wasafirishaji Watalii Tanzania (TATO) imeandaa mafunzo haya ili kuboresha huduma na kuongeza ushindani wa kimataifa," alieleza.


Alisema mafunzo hayo yanaendana na malengo ya Serikali ya kufikia watalii milioni 8 na kuongeza mchango wa utalii katika Pato la Taifa hadi asilimia 20 ifikapo mwaka 2030.


Katika mafunzo hayo yenye kaulimbiu isemayo "Utaalamu, Usalama na Uongoza Watalii Wenye Uwajibikaji katika Maeneo ya Hifadhi Tanzania,'" washiriki wanatarajiwa kuimarisha taaluma zao, kuongeza uelewa wa masuala ya usalama na kuboresha utoaji wa huduma kwa viwango bora vya kimataifa.


Dkt. Kijaji alisisitiza kuwa Tanzania ina ushindani mkubwa katika soko la kimataifa la utalii, hivyo ni lazima huduma zinazotolewa ziendane na hadhi ya nchi hiyo inayojulikana kama "Kituo Bora cha Safari za Utalii Duniani".

Aidha, aliwakumbusha waongoza watalii umuhimu wa kuzingatia usalama wa wageni, hasa wanapokuwa katika hifadhi za taifa, akieleza kuwa wanabeba dhamana kubwa ya maisha ya watalii.


"Ni lazima muwe na uwezo wa kufanya maamuzi ya haraka na sahihi kila wakati Kuzingatia taratibu za hifadhi si tu kunalinda wageni, bali pia kunahifadhi rasilimali zetu kwa vizazi vijavyo". alisisitiza.


Waziri huyo alibainisha kuwa jumla ya waongoza watalii 2,000 wanashiriki mafunzo hayo kati ya 13,050 waliosajiliwa, akiwataka washiriki kuwa mabalozi wa maarifa kwa wenzao watakaokosa fursa hiyo.


Pia aliwakumbusha kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya kazi hiyo, ikiwa ni pamoja na kumiliki leseni halali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Katika hatua nyingine, Dkt. Kijaji alisema.


Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa matukio makubwa ya kimataifa, yakiwemo Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) Oktoba 2026, Fainali Kuu za Tuzo za Utalii Duniani (World Travel Awards Grand Final 2026) pamoja na mashindano ya AFCON 2027.


Alisema matukio hayo ni fursa adhimu kwa sekta ya utalii, hivyo aliwataka wadau kuanza maandalizi mapema kwa kubuni vifurushi maalum vya utalii vitakavyowavutia wageni watakaohudhuria matukio hayo.


"Ni muhimu kuvitangaza mapema ili wageni wajue kuwa wanapokuja kushiriki matukio haya, pia wanapata nafasi ya kipekee ya kutembelea vivutio vya Tanzania". alisisitiza.


TATO: LENGO YA PROGRAMU HII NI KUWANOA VIJANA ILI WAWEZE KUKABILIANA NA MSIMU MPYA WA UTALII KIMATAIFA.


Kwa upande wake, Chama cha Waendeshaji wa Utalii Tanzania (TATO), ambacho ndicho waandaaji wa mafunzo kwa waongoza watalii na madereva wa watalii, kimesema lengo la programu hiyo ni kuwajengea uwezo na kuwanoa vijana ili wawe tayari kukabiliana na msimu mpya wa utalii nchini, sambamba na kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la kimataifa.

Akizungumza kwa niaba ya TATO, Mkurugenzi Mtendaji wake, Elirehema Maturo, alisema mafunzo hayo yaliyofunguliwa na waziri wa Maliasili na Utalii ,Ashatu Kijaji jijini Arusha.


Mafunzo hayo yanatajwa kuwanufaisha wadau wa utalii wapatao 2,000 nchini, wakiwemo waongoza watalii na madereva, hatua ambayo ni muhimu katika kuinua ubora wa huduma katika sekta hiyo nyeti.


Alisema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka, yakiwa sehemu ya mkakati wa kuboresha ubora wa huduma kwa kujifunza kutokana na changamoto zilizojitokeza katika misimu iliyopita 'Utalii ni biashara ya kimataifa, na kama hatutakuwa na ushindani wa kutosha tutapoteza nafasi yetu sokoni.


"Hivyo ni lazima tuendelee kuboresha ubora wa huduma kila wakati," alisema Maturo.

Aliongeza kuwa mafunzo hayo pia ni jukwaa muhimu la wadau kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto za kiutendaji hususan katika kipindi cha msimu wa chini wa utalii (low season), hali inayosaidia kuimarisha mikakati ya sekta hiyo.


Maturo amesisitiza kuwa TATO itaendelea kuandaa na kuratibu mafunzo kama haya, na pia inahitaji mafunzo hayo kupanuliwa kufika katika mikoa mingine nchini ili kuinua viwango vya huduma kitaifa.


Alihitimisha kwa kusisitiza kuwa ubora wa huduma ndiyo msingi mkuu wa ushindani wa Tanzania katika sekta ya utalii kimataifa, akibainisha kuwa wageni wanaokuja nchini wanapaswa kuondoka wakiwa mabalozi wazuri wa Tanzania duniani.


ZARA: TUPO TAYARI KUHAKIKISHA TAIFA LETU LINAZIDI KUKUA KIUTALII PANDE ZOTE ZA ULIMWENGU NA TUNAISHUKURU SERIKALI KUZIDI KUTUWEKEA MAZINGIRA MAZURI YA KIBIASHARA.


KAMPUNI ya utalii ya Zara Tours, mojawapo ya kampuni zinazoongoza katika sekta ya utalii Tanzania, imeendelea kuonesha mchango wake kubwa katika kukuza ubora wa huduma na kuimarisha taswira ya nchi katika soko la kimataifa la utalii, huku ikiiunga mkond juhudi za Serikali katika kuboresha sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa.

Akizungumza kwa niaba ya kampuni hiyo, jijini Arusha, Mkurugenzi wa Zara Tours, Zainab Ansell ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa juhudi zake za makusudi katika kuimarisha sekta ya utalii, akisema mafanikio yanayoendelea kuonekana yanatokana na ushirikiano thabiti kati ya Serikali na sekta binafsi.


Alisema Zara Tours inajivunia kuwa sehemu ya maendeleo ya sekta hiyo kupitia uwekezaji wake katika kuboresha huduma, kutoa mafunzo kwa watumishi, na kuhakikisha wageni wanaopata huduma zao wanabaki kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania duniani.


"Hii ni hatua kubwa sana kwa sekta yetu Tunapoongelea utalii bora, tunamaanisha kuwaandaa wale wanaokutana moja kwa moja na wageni wetu. Mafunzo haya yanakwenda kuboresha kwa kiwango kikubwa ubora wa huduma na taswira ya nchi yetu," alisema Zainabu.


Aliongeza kuwa kampuni hiyo itaendelea kushiriki kikamilifu katika juhudi za kitaifa za kuinua ubora wa utalii, hususani kupitia mafunzo na ubunifu wa hudumabzinazokidhi viwango vya kimataifa, akisisitiza kuwa uwekezaji katika rasilimali watu ni msingi muhimu wa mafanikio ya sekta hiyo.



Comments