MBUNGE WA UINGEREZA BADO VITUO 3 KUFIKA KILELE CHA MLIMA KILIMANJARO.

Mbunge wa Uingereza bado vituo vitatu afike kileleni Mlima Kilimanjaro.

Mwandishi wetu, Kilimanjaro.


Mbunge wa Bunge la Uingereza, Tracey Crouch anaendelea kupanda Mlima Kilimanjaro na Leo amefika kituo cha Moyr Hut mita takriban 4600 kutoka usawa wa bahari akibakiza vituo vitatu kufika kileleni na kuweka historia .

 Crouch anapanda Mlima Kilimanjaro,akiwa na wanawake wenzake wanane kupitia kampuni ya Big Expedition and Safaris ya jijini Arusha na tangu ameanza kupanda amekuwa na furaha na kubwa kupanda Mlima huku akifurahia kukaribia kileleni mwa Mlima Kilimanjaro.


Mbunge huyo ambaye yupo katika kampeni ya kuchangisha fedha kufanikisha matibabu ya Saratani ya Matiti kwa wagonjwa kesho anatarajiwa kufika kituo cha Baranko.

 

Crouch ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Michezo wa Uingereza kati ya mwaka 2017/18 anatarajiwa kushuka Mlimani Agosti 5 na kupokewa na wadau mbalimbali wa Utalii 


 kampuni ya kimataifa ya Utalii ya Uingereza ya Action Challenge kwa kushirikiana na Big Expedition and Safaris ndio wanampandisha kileleni Mbunge huyo na wenzake katika safari iliyopewa jina la Delux VIP ambapo wanaopanda mlima wanapewa huduma za viwango vya juu zaidi (VIP service).


Mbunge huyo, ameanza Julai 29,2023 kupanda mlima huo mrefu barani Afrika, kupitia njia ya Lemosho .


Mkurugenzi wa kampuni ya Big Expedition and Safaris, Angel Minja akizungumza na MAIPAC media amesema ujio wa Mbunge huyo wa Uingereza ni kazi nzuri ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya The Royal Tour.


"Wageni kama Hawa kuwapata sio rahisi hivyo tunampongeza Sana Mama Rais Samia kuendelea kutangaza Utalii wetu vizuri"amesema.

Minja pia ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii, Waziri Mohamed Mchengerwa na Katibu Mkuu Dk Hassan Abbas na wasaidizi wao kwa kazi nzuri wanayofanya kuboresha Utalii.


"Waziri wetu anafanya kazi nzuri na sisi kama wamiliki wa kampuni za Utalii tunampongeza na tunamuunga mkono"amesema.


Minja amesema kampuni yao ambayo mwaka huu imetimiza miaka 20 tangu kuanzishwa imekuwa na mafanikio hasa kutokana na kuweza kupokea wageni wengi maarufu Duniani.


"Sisi pia tunajitahidi sana kutoa huduma bora zenye viwango vya kimataifa na nzuri kwa wageni ndio sababu wageni maarufu Duniani wanapitia kampuni yetu ambayo ni ya wazawa"amesema.


Amesema hivi karibuni walipokea wageni ambao ni mabalozi wa Utalii kutoka nchini Uingereza lakini pia familia za watoto wa viongozi wakubwa katika Mataifa yaliyoendelea wamekuwa wakitumia kampuni yao.

Comments