WAZIRI MKUU MAJALIWA, AWATAKA WADAU WA MAENDELEO YA AFYA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KATIKA KUFANIKISHA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA BIMA YA AFYA..

🔴ASEMA SERIKALI IMESHA ANZA MPANGO WA KUONGOZA BAJETI KATIKA SEKTA YA AFYA.

 

Na Lucas Myovela - Arusha.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Washirika wa Maendeleo kushikiriana na Serikali katika kufanikisha utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote na kusaidia kuimarisha mfumo wa ugharamiaji huduma za afya ili kuufanya kuwa endelevu.

Mheshimiwa Majaliwa amesema ili kuimarisha mfumo wa ugharamiaji wa huduma za afya Serikali tayari imeanza kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuendelea kuongeza kiwango cha bajeti ya Sekta ya Afya.

 

Ametoa wito huo leo Oktoba 30, 2024, alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa mdahalo wa Bima ya Afya kwa Wote na Jukwaa la Kitaifa la Ugharamiaji wa Huduma za Afya kwa ajili ya utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote (Universal Health Insurance - UHI), jijini Arusha.

“Pia, tumeanzisha mfuko kwa ajili ya kugharimia wananchi wasio na uwezo, tumebainisha vyanzo mahsusi vya fedha kwa ajili ya kugharimia Bima ya Afya kwa wananchi wasio na uwezo ambapo katika bajeti ya mwaka 2024/2025 zimetengwa shilingi bilioni 173.5 kwa madhumuni hayo.” Amesema Majaliwa 

 

Aidha Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote utafanikiwa kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika sekta ya afya ikiwemo ujenzi wa miundombinu na uborashaji wa huduma za uchunguzi.

 

Ameeleza kuwa Serikali imewekeza katika ununuzi na usimikaji wa vifaa tiba vya kisasa vya uchunguzi na ugunduzi wa magonjwa mbalimbali, ambapo hadi sasa zipo mashine za MRI 13, CT-Scan 45, Digital X-Ray 346 na Ultrasound 668 kutoka 476 zilizokuwepo mwaka 2021. “Hatua hii imewezesha kupatikana kwa huduma za kibingwa za uchunguzi.”

 

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali imeendelea kuimarisha hali ya upatikanaji wa dawa nchini kwa kutoa fedha kila mwezi kwa ajili ya ununuzi wa dawa. 

“Hadi kufikia Oktoba 2024 upatikanaji ulikuwa umefikia wastani wa asilimia 85 ambapo kwa upande wa zahanati ni asilimia 76, vituo cha afya ni asilimia 75, Hospitali za Halmashauri asilimia ni 78, Hospitali za Rufaa za Mikoa ni asilimia 99 na Hospitali ya Taifa, Maalum na kanda ni asilimia 98”. Ameeleza majaliwa.




Comments