DKT. BITEKO ATAKA WATAFITI NA WABUNIFU NCHINI WATAMBULIWE ILI ULETA MAENDELEO.

🔻ATAKA WATAFITI WAENDELEZWE KITAALUMA PASIPO KUVUNJWA MOYO.

Posted by: Lucas Myovela.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema umefika wakati kwa Serikali na taasisi na Mashirika kutambua, kuthamini na kutumia tafiti za wanasayansi wa ndani ya nchi ili kutatua changamoto zilizopo.

DKt. Biteko amemsema hayo leo Disemba 2, 2024 wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua Kongamano la tisa la Sayansi, Teknolojia, Ubunifu na maonesho linaloendelea Jijini Dar es Salaam.


Amesema wanasayansi nchini wanafanya kazi nzuri na kubwa ya kutafuta suluhu ya matatizo mbalimbali katika jamii lakini kazi zao zinatambuliwa zaidi nje ya nchi kuliko zinavyotambuliwa nchini jambo ambalo linaweza kuwavunja moyo.

“Kongamano hili ni la kujadili na kutafuta suluhu ya matatizo tuliyonayo, tutumie tafiti za wanasayansi wa ndani badala ya kuwavunja moyo na kila anayejaribu kwa kutafiti apewe fursa ili aendelee kutafiti zaidi na matokeo tutayaona,” amesema DKt. Biteko.


Ameongeza kuwa Serikali inatambua mchango wa wanasayansi na kuwawezesha watafiti na wabunifu na kupitia Tume  ya Sayansi na Teknolojia COSTECH imetoa kiasi cha bilioni 32 kwa ajili ya kuimarisha miradi ya utafiti na ubunifu.


Tangu mwaka 2015 Serikali imeshapokea kiasi cha shilingi bilioni 222.8 kwa ajili ya kujenga uwezo kwa wanasayansi wabunifu kuendeleza miradi mbalimbali ambazo zimesaidia kuwajengea uwezo wanasayansi wakiwemo wanasayansi vijana.

Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia. Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali imeanza kutambua jitihada za Wanasayansi, Watafiti wa ndani ya nchi na baadhi yao wametunukiwa vyeti kwa kutambua mchango wao kwa maendeleo yaliyofikiwa katika sekta mbalimbali ikiwemo Afya, Kilimo na Uvuvi.


Amefafanua kuwa njia moja yakufanya jitihada hizo kuwa endelevu, Serikali imeanzisha mfuko wa mikopo nafuu wa kubiasharisha bunifu na tafiti Tanzania unaojulikana kama Samia Fund.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu ameishukuru Serikali kwa uwezeshaji ambao umeiwezesha kutekeleza majukumu yake kwa viwango na kuwa moja ya taasisi mahiri ya kupigiwa mfano Kusini mwa Jangwa la Sahara.


Ameongeza kuwa COSTECH kupitia program mbalimbali imewasaidia vijana wengi kubadili ndoto zao kuwa fursa ambapo pamoja na mambo mengine imefikia uwezo wa kutoa vibali 1000 kwa watafiti kutoka nje ya nchi.

Balozi wa Norway nchini, Mhe. Tine Tonnes ameipongeza Tanzania kufuatia hatua zake za kuendeleza watafiti na wabunifu huku akieleza utayari wa nchi hiyo kuendelea kuunga mkono program za uhifadhi wa mazingira.


Vikundi 19 vimepokea mfano wa hundi ya shilingi Bilioni 6.3 ikiwa ni mkopo kwa watafiti, wabunifu waliofanya kazi inayosababisha matokeo.




Comments