SASA NI ODERO NA LISSU KUPANGUA MASWALI YA CHIF ODEMBA.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) taifa na mgombea wa nafasi ya hiyo kwenye uchaguzi unaoendelea ndani ya chama hicho, Freeman Mbowe @freemanmbowetz amekacha mdahalo uliokuwa umeandaliwa na kituo cha runinga cha Star TV ambao unafanyika usiku wa leo Jijini Dar es Salaam.
Kituo cha Star TV kupitia kwa mwandaaji wa mdahalo huo Edwin Odemba @chiefodemba amesema kwa wiki kadhaa sasa amefanya jitihada za kila aina kumtafuta Mwenyekiti Freeman Mbowe kwa ajili ya kupata uthibitisho wake kushiriki mdahalo huo pasipo mafanikio.
Hata mara baada ya kuona imekuwa ngumu kumpata Freeman Mbowe kwa ajili ya kuthibitisha kushiriki mdahalo huo, Odemba aliamua kumtafuta Katibu Mkuu wa chama hicho John Mnyika @jjmnyika kwa ajili ya kusaidia kumpata Mwenyekiti Mbowe ili athibitishe kuhudhuria mdahalo, hata hivyo Mnyika amesisitiza kuwa suala la mdahalo ni la mgombea binafsi, hivyo waandaaji wamtafute Freeman Mbowe mwenyewe.
Taarifa za kuaminika kutoka kwa wandani wa Freeman Mbowe zinaeleza kuwa Mbowe amekacha mdahalo huo kwa kile anachoamini kuwa kufanya hivyo ni ‘kubagaza’ chama.
Mgombea Tundu Lissu @TunduALissu kupitia ukurasa wake wa X amethibitisha kushiriki mdahalo huo na amesema mdahalo kwa wagombea ni utamaduni wa kisiasa unaopaswa kujengwa na kukuzwa kama sehemu ya ujenzi wa demokrasia nchini Tanzania.
Kwa upande wake mgombea Odero Charles Odero ameiambia Jambo TV kuwa atashiriki mdahalo huo, na hakika Jambo Tv tutakuletea mdahao huo mbashara.
"Tukutane kwenye Medani Kuu Live na Chief Edwin Odemba kujadiliana juu ya 'Uongozi Wetu na Hatma ya CHADEMA 2025 & Beyond'! Katika kuelekea 'Fainali' ya tarehe 21 Januari, 'Mdahalo wa Wenyeviti' ni utamaduni wa kisiasa unaopaswa kujengwa na kukuzwa kama sehemu ya ujenzi wa utamaduni wa kidemokrasia katika nchi yetu na chama chetu. Ingependeza sana kama tungekuwa wote watatu, but haya ni mambo mapya kwetu na yana hofu zake...!"Ameandika Lissu.
Comments
Post a Comment