TANZANIA YAIMARISHA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA YA NYUKLIA KATIKA AFYA KILIMO NA NISHATI.
Akizungumza katika tukio hilo, Profesa Najat amesema kwa sasa TAEC inasimamia na kuratibu utekelezaji wa miradi mikubwa minne ya kimkakati inayotekelezwa kwa kushirikiana na Serikali na wadau wa kimataifa, ikiwemo IAEA.
Ameeleza kuwa mradi wa kwanza unalenga uboreshaji wa mbegu na tija ya kilimo kwa kutumia teknolojia ya nyuklia, unaotekelezwa katika eneo la Nelson Mandela - Arusha, kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao bora na yenye ustahimilivu kwa wakulima wa Tanzania.
Ameeleza kuwa mradi wa kwanza unalenga uboreshaji wa mbegu na tija ya kilimo kwa kutumia teknolojia ya nyuklia, unaotekelezwa katika eneo la Nelson Mandela - Arusha, kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao bora na yenye ustahimilivu kwa wakulima wa Tanzania.
Mradi wa pili ni wa ujenzi wa maabara ya kisasa ya mifugo Zanzibar, unaotekelezwa kwa ushirikiano na maabara kutoka Vietnam, ukiwa na lengo la kuboresha uchunguzi wa magonjwa ya wanyama kuimarisha usalama wa chakula na kukuza sekta ya mifugo kwa kutumia sayansi ya kisasa.
Profesa Najat amesema mradi wa tatu ni wa ujenzi wa kituo cha Irradiator jijini Dar es Salaam, ambacho kitahusika na matumizi ya mionzi kwa ajili ya kuhifadhi vyakula, kuua vimelea na kuongeza muda wa matumizi ya mazao bila kuhatarisha afya za walaji.
Akizungumzia mradi wa nne, Profesa Najat amesema ni mradi mkubwa zaidi unaolenga kuimarisha huduma za tiba na uchunguzi wa saratani nchini.
Amesema awali Tanzania ilikuwa na vituo viwili pekee vya huduma hizo ambavyo ni Hospitali ya Ocean Road na Bugando, lakini kupitia mradi huo idadi ya vituo itaongezeka kutoka viwili hadi sita.
Vituo vipya vitakavyotoa huduma hizo ni pamoja na KCMC, kinachotarajiwa kuanza kutoa huduma hivi karibuni, Hospitali ya Benjamin Mkapa, ambayo ujenzi wake uko katika hatua za mwisho, pamoja na Kituo cha Mbeya, ambacho nacho kipo katika hatua za utekelezaji.
Ameongeza kuwa ujumbe wa IAEA umetembelea pia maeneo mbalimbali ya miradi, ikiwemo Hospitali ya Benjamin Mkapa, na unatarajiwa kuendelea na ziara katika Shinyanga na Zanzibar ambapo wageni hao wameeleza kufurahishwa na maendeleo makubwa yaliyofikiwa na Tanzania katika sekta ya nyuklia kwa matumizi ya amani.
"Wageni wetu wametambua tofauti kubwa kati ya hali ya sasa na miaka ya nyuma. Leo tuna miundombinu imara, maabara za kisasa na wataalamu waliobobea, jambo linaloonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Tanzania katika kuwekeza kwenye sayansi na teknolojia,' Amesema Profesa Najat.
Amesema pia TAEC kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati imeendelea kufanya mazungumzo ya kitaalamu kuhusu maandalizi ya muda mrefu ya matumizi ya nishati ya nyuklia kama chanzo mbadala cha umeme, hatua inayolenga kuimarisha usalama wa nishati na kukuza uchumi wa taifa.
Profesa Najat, amesisitiza kuwa jitihada hizo zinaakisi dhamira ya Serikali ya kuendelea kuwekeza katika sekta ya afya sayansi na teknolojia, huku TAEC kiendelea kusimamia miradi hiyo kwa uwazi na ufanisi kwa manufaa ya watanzania.








Comments
Post a Comment