WAZIRI KIKWETE AWATAKA WADAU WA KINGA JAMII KUYAISHI MAELEKEZO YA RAIS DKT. SAMIA, KUFIKIA DIRA YA TAIFA 2050 KUFIKIA MAISHA BORA NA USTAWI WA WOTE.

🔺️WADAU WAHAMASISHWA KUTEKELEZA SERA YA KINGA YA JAMII.

Na Lucas Myovela - Arusha.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimeti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, amewataka wadau wa sekta ya Kinga ya Jamii kujipanga vyema na kuweka nguvu katika kutekeleza Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii ilikufikia malengo yaliyokusudiwa.

Waziri Kikwete, amesema Sera hiyo imeonyesha mwelekeo wa Sekta ya Kinga ya Jamii nchini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa wananchi wote wenye uwezo wa kuzalisha kipato wanajiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.


Kikwete amesema hayo leo Februari 10,2026 wakati akifunga Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Kinga ya Jamii uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Arusha (AICC).

Amesema kuwa ndoto ya Watanzania ni kuwa ndani ya mfumo wa hifadhi ya jamii kitu ambacho kwa sasa inakwenda kukamilika kutokana na uwepo wa Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii.


"Nipende kuipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi nzuri ya kuandaa sera hii muhimu kuhusu kinga ya jamii kitu ambacho kinakwenda kuwa na mafanikio makubwa katika taifa ketu kwasasa kila mwananchi anao uwezo wa kujiunga na mifuko hii kwa ajili ya kujiwekea akiba na kujinga na majanga mbali mbali.


"Napenda kutoa wito kwa wadau wote wa sekta ya Kinga ya Jamii kuyaishi maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo aliyatoa wakati wa kuhitimisha Bunge la 12, tarehe 27 Juni 2025 kuhusu utekelezaji wa sera hii pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo lengo la pili linasisitiza Maisha Bora na Ustawi wa Wote". Amesema Kikwete.

Aidha ameeleza kuwa mpaka sasa maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yameleta mafanikio makubwa katika sekta hiyo ambayo yameifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 17 zenye utaratibu bora wa kinga ya jamii.

Awali Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Bi, Mary Maganga, amesema Mkutano huo wa siku mbili umetoa fursa kwa wadau kujadili kwa kina na kubadilishana uzoefu katika kuboresha sekta hiyo kwa ajili ya maendeleo ya taifa.


"Mkutano huu ulilenga kukuza uelewa wa umma kuhusu umuhimu wa kinga ya jamii sambamba na kuendeleza ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wengine ili kuimarisha sekta ya kinga ya jamii nchini," amesema.


Mkutano huo wa wadau wa Sekta ya Kinga Jamii ulizindiliwa Februari 9,2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Clement Sangu, Kwa niba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Ambapo alieleza kuwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya kinga ya jamii nchini ambapo thamani ya mifuko yote ya hifadhi ya jamii imeongezeka maradufu kutoka shilingi trilioni 10.43 mwaka 2020 hadi kufikia shilingi trilioni 24.20 mwezi Desemba 2025.







Comments