LHRC YAITAKA SERIKALI KUREKEBISHA KANUNI ZA MAUDHUI MTANDAONI

đź’˘WAAHIDI KUENDELEA KUPAMBANIA HAKI ZA WANAHABARI NA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI KWA KADRI WAWEZAVYO IKIWEMO KUFUNGUA KESI MAHAKAMANI.

Na Lucas Myovela - Arusha.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeiomba Serikali kufanya marekebisho ya haraka ya kanuni zinazosimamia maudhui mtandaoni, kikieleza kuwa baadhi ya vifungu vyake vinakinzana na misingi ya haki ya kusikilizwa na vinaweza kudhoofisha uhuru wa vyombo vya habari nchini.

Wito huo umetolewa Jijini Arusha wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari, ambapo Meneja wa Uchechemuzi wa LHRC, Raymond Kanegene, amesema ni muhimu sheria na kanuni hizo ziendane na Katiba pamoja na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.


Amesema LHRC, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imekuwa ikichukua hatua za kisheria ndani na nje ya nchi kulinda haki za msingi, ikiwemo uhuru wa kujieleza na kupata habari. Miongoni mwa hatua hizo ni kufungua kesi za kimkakati kupinga baadhi ya vipengele vya Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni za mwaka 2020 na 2022.


Kwa mujibu wa Kanegene, mojawapo ya kesi hizo ilifunguliwa katika Mahakama ya Afrika Mashariki pamoja na mahakama za ndani, ikilenga kupinga vifungu vinavyodaiwa kukiuka haki za msingi, hususan haki ya mtu kusikilizwa kabla ya kuchukuliwa hatua dhidi yake.


Alisema changamoto kubwa ipo kwenye utaratibu unaotumika na Kamati ya Maudhui ya Mtandaoni, ambapo baadhi ya wahusika wamekuwa wakichukuliwa hatua bila kupewa nafasi ya kujitetea.


“Kanuni za haki za asili zinataka kila mtu apewe nafasi ya kusikilizwa kabla ya kuamuliwa. Kutokuwepo kwa nafasi hiyo ni kinyume na misingi ya haki,” amesema.


Aidha, amekumbusha kuwa Mahakama ya Rufaa ilishawahi kutoa uamuzi unaobainisha kasoro katika baadhi ya vifungu vya kanuni hizo, ikivitaja kuwa vinakiuka masharti ya Katiba, hususan Ibara ya 13 inayohusu haki ya kupata haki sawa.


Hata hivyo, amesema pamoja na uamuzi huo, bado marekebisho hayajafanyika, hali inayochangia kuendelea kwa malalamiko kutoka kwa wadau wa sekta ya habari kuhusu kufungiwa au kusimamishwa kwa vyombo bila kufuata utaratibu wa haki.


Kutokana na hali hiyo, LHRC imesisitiza umuhimu wa Serikali kuchukua hatua za makusudi kurekebisha kanuni hizo ili kuimarisha uwajibikaji, kulinda haki za msingi na kuweka mazingira rafiki kwa vyombo vya habari kufanya kazi kwa uhuru.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania, Musa Juma, amesema bado kuna changamoto kubwa katika sekta ya habari nchini, akisisitiza umuhimu wa kurekebisha sheria zenye mapungufu ili kuwawezesha waandishi kutekeleza majukumu yao kwa uhuru.


Amesema waandishi wanapokabiliwa na vikwazo mbalimbali hushindwa kuwa wabunifu, huku akisisitiza pia umuhimu wa kuboresha maslahi yao ili kuongeza weledi na ufanisi kazini.


Aidha, amewataka wamiliki wa vyombo vya habari kuboresha maslahi ya waandishi, akibainisha kuwa mazingira bora ya kazi ni msingi wa ubunifu na utoaji wa habari zenye ubora.

Comments