MIKA 42 BAADA YA SOKOINE: WANANCHI WASEMA CHANGAMOTO ZA UONGOZI NA UZALENDO WA VIJANA ZINAIBUA MASWALI MAPYA.

 πŸ”Ί️WAZEE WAFUNGUKA, WADAI CHANGAMOTO KUBWA KWASASA NI KUPUNGUA NIDHAMU KWA WATUMISHI WA UMMA NA VIJANA KUKOSA MUAMKO WA UZALENDO KWA TAIFA.

Na Lucas Myovela-Monduli – Arusha.
April 10, 2026.

Miaka 42 baada ya kufariki kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani, Hayati Edward Moringe Sokoine, wananchi wa mkoani Arusha wanasema urithi wake wa uadilifu na uzalendo bado unakumbwa na changamoto katika kizazi cha sasa, hususan kwa baadhi ya vijana na viongozi wapya.

Wakizungumza wakati wa maandalizi ya misa ya kumbukizi itakayofanyika Aprili 12 katika eneo la Monduli Juu, wananchi hao wamesema pamoja na kumbukumbu ya mafanikio ya Sokoine, bado kuna pengo kubwa la uongozi wa kuwajibika na uzalendo wa vitendo.


Baadhi ya wazee kutoka Chama cha Wazee Wanaume Tanzania wamesema changamoto kubwa ya sasa ni kupungua kwa nidhamu ya utumishi wa umma, pamoja na baadhi ya vijana kukosa mwamko wa uzalendo wa kweli kwa taifa.


Akizungumza, Joseph Laitatei, Makamu wa Rais wa chama hicho, amesema Sokoine alikuwa mfano wa kiongozi aliyekuwa karibu na wananchi na asiyeogopa kuchukua maamuzi magumu kwa maslahi ya taifa.


Kwa upande wake, Cloud Gwangu, mkazi wa Arusha, amesema kizazi cha sasa kinakabiliwa na changamoto ya kupungua kwa ari ya kazi na uzalendo wa vitendo, hali inayohitaji marekebisho ya kimtazamo.


“Vijana wengi leo hawana ule moyo wa kujitoa kama ilivyokuwa zamani. Sokoine alikuwa mfano wa kazi, si maneno,” amesema Gwangu.


Abel Mollel, Mwenyekiti wa Wilaya wa chama hicho, amesema changamoto ya uwajibikaji katika taasisi mbalimbali inahitaji viongozi wenye msimamo kama wa Sokoine, ili kurejesha imani ya wananchi.


Geoge Mwakalukwa naye amesema uongozi wa sasa unahitaji kujifunza kuwa uzalendo si maneno ya kisiasa bali ni matendo ya kila siku.


Aidha, viongozi hao wameipongeza familia ya Sokoine kwa kuendelea kudumisha kumbukumbu yake kila mwaka, wakisema hatua hiyo inasaidia kuwaelimisha vijana kuhusu historia ya uongozi bora na maadili ya taifa.Hayati Sokoine alifariki dunia Aprili 12 mwaka 1984 kufuatia ajali ya gari iliyotokea Dumila.


Wananchi wamesema licha ya kupita kwa miongo minne, mjadala kuhusu uongozi bora, uzalendo na uwajibikaji bado ni muhimu zaidi kwa kizazi cha sasa.


Mwisho

Comments