DCEA, PSSSF NA NSSF WAWAFIKIA WARAIBU WA MADAWA YA KULEVYA.

đź’˘WATOA VITANDA NA MAGODORO 160 KWA NYUMBA ZATE WARAIBU.

đź’˘MSAADA HUO WALENGA KUWAREJESHA WARAIBU KATIKA HALI ZAO ZA KAWAIDA.

Na Lucas Myovela - Arusha.

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), wametoa vitanda 160 pamoja na magodoro 160 vyenye thamani ya sh, milioni 43 kwa ajili ya kusaidia waraibu wa dawa za kulevya wanaopata huduma katika nyumba za upatikanaji nafuu (Sober House) zinazoratibiwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kaskazini.

Akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Dk, Rhino Nyansaho, mwakilishi wa mfuko huo, Venance Mwaijibe,alisema  msaada huo uliokabidhiwa   jana Jijini Arusha katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na wadau wa mapambano dhidi ya dawa za kulevya. 


Alisema PSSSF imeamua kuunga mkono juhudi za serikali kwa kutoa vitanda na magodoro hayo ili kuboresha huduma za malazi kwa waraibu wanaopatiwa matibabu na ushauri nasaha kwani mfuko huo unaamini katika kushirikiana na jamii kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.


“PSSSF tuna kauli mbiu ya ‘Leo, Kesho’. Kwa kushirikiana na NSSF tunajenga maisha ya sasa na ya baadaye, tumeungana kurejesha kwa jamii sehemu ya faida tunazopata kwa kusaidia mapambano dhidi ya dawa za kulevya ili kupata raia wema na wenye mchango chanya kwa taifa,” . 


Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Abubakar Mshangama, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo, Masha Mshomba, alisema mifuko hiyo miwili imeamua kushirikiana kuunga mkono juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

Naye Sarah Ndaba, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa DCEA, Aretus Lyimo aliishukuru PSSSF na NSSF kwa msaada huo, akisema utasaidia kuimarisha huduma zinazotolewa kwa waraibu wanaopata nafuu kupitia nyumba hizo.


“Msaada huu utasaidia waraibu kurejea katika hali zao za kawaida. Tunaomba wadau wengine wajitokeze kusaidia juhudi hizi kwa kuwa mazingira bora ya matibabu yanaongeza uwezekano wa mgonjwa kupona na kurejea katika maisha ya kawaida,” 

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha,  Amos Makalla, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, alisema mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanawezekana kupitia ushirikiano wa wadau mbalimbali. 


Alisema DCEA inaendelea kudhibiti biashara ya dawa za kulevya pamoja na kuhakikisha huduma za matibabu zinapatikana katika vituo mbalimbali.


“Ni lazima tulinde nguvu kazi ya taifa kwa maendeleo endelevu.


 Tunawashukuru wadau wetu PSSSF na NSSF kwa kusaidia kuboresha mazingira katika nyumba zaidi ya 19 zinazohudumia waraibu 505, wakiwemo wanawake 98 na wanaume 407,” alisema Mkude.


Kwa upande wake, mwakilishi wa Sober House, Samson Karume, alisema nyumba hizo si sehemu za kuwaficha waraibu, bali ni vituo vya kuwasaidia kurejea katika maisha ya kawaida kupitia ushauri nasaha, matibabu na malezi maalum.


Alisema nyumba zaidi ya 19 zinatoa huduma hizo kwa waraibu waliotoka katika mazingira magumu, wakiwemo vijana waliokuwa wamepoteza mwelekeo wa maisha, wasomi na hata watoto wa viongozi mbalimbali


Karume alitaja changamoto zinazoikabili Sober House kuwa ni pamoja na jamii kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu waraibu waliopona, ukosefu wa ajira kwa waraibu waliorejea katika hali ya kawaida kutokana na jamii kuwaamini bado wanatumia dawa, ukosefu wa ufadhili unaosababisha baadhi ya nyumba kufungwa, pamoja na uhaba wa wataalamu wa afya ya akili huku nyumba tatu zikifungwa kutokana na ukosefu wa msaada wa kifedha.


Huku baadhi ya waraibu waliopona , Baita Chacha, alisema alitumia dawa za kulevya kwa miaka 15 kabla ya kupata msaada kupitia Sober House, ambapo sasa amepona baada ya kuishi katika kituo hicho kwa mwaka mmoja kwani uraibu ni changamoto ya afya ya akili inayohitaji msaada wa karibu kutoka kwa jamii na wataalamu


“changamoto ya uraibu, akieleza kuwa wengi wao hawakuingia katika matumizi ya dawa za kulevya kwa makusudi bali walikumbwa na mazingira magumu ya maisha".













Comments