💢WAHIDHINISHA PENDEKEZO LA GAWIO LA SHILINGI 90 KWA KILA HISA IKIWA NI ONGEZEKO LA LA 38% KULINGANISHA NA SHILINGI 65 ZILIZO TOLEWA MWAKA 2025.
Na Lucas Myovela - Arusha.
Wanahisa wa Benki ya CRDB wamepitisha kwa kishindo ripoti ya Wakurugenzi pamoja na Taarifa za Hesabu Zilizokaguliwa kwa mwaka 2025 na wameidhinisha pendekezo la gawio la Shilingi 90 kwa kila hisa, ikiwa ni ongezeko la asilimia 38 ikilinganishwa na shilingi 65 zilizotolewa mwaka 2025, Pamoja na Kupitisha azimio la kuiteua Kampuni ya Ukaguzi wa Hesabu ya nje ya PWC kuwa wakaguzi wa Benki kwa mwaka 2026.
Maadhimio hayo yamefanyika leo Mai 16, 2025 Jijini Arusha katika mkutano wa 31 wa wanahisa wa benki hiyo ambayo kwa asilimia kubwa inamilikiwa na wanahisa na kuweka mikakati kabambe ya kuzidi kukua kiuchumi na kuwavutia vijana katika uwekezaji.
Aidha wanahisa wameadhimia kwa pamoja Mkutano Mkuu ujao wa 32 kufanyika tareh 15 Mei 2027 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Arusha (AICC) na kuhamasisha vijana ambao bado hawajawekeza katika Benki hiyo waone kuwa huu ndiyo wakati wa kufanya maamuzi sahihi.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Abdulmajid Mussa Nsekela, amesema kuwa mwaka 2025 Benki hiyo iliendelea kuimarisha nafasi yake kama taasisi kubwa zaidi ya kifedha nchini kupitia ukuaji mkubwa wa biashara, ubunifu wa kidijitali na upanuzi wa huduma zake za kikanda.
Akiwasilisha taarifa yake, Dkt. Nsekela, alisema jumla ya mali za Benki ziliongezeka kwa asilimia 33.6 hadi kufikia Shilingi trilioni 22.3, huku mikopo na advances zikifikia Shilingi trilioni 13.7, hatua aliyosema inaonyesha uwezo wa Benki kuendelea kuchochea ukuaji wa sekta mbalimbali za uchumi hapa nchini na nje ya nchi.
Amesema Benki ya CRDB itaendelea kuwekeza katika teknolojia, ujumuishaji wa kifedha na huduma zinazounganisha uzoefu wa kidijitali na huduma za ana kwa ana ili kuongeza ushindani, kuboresha uzoefu wa wateja na kujenga thamani endelevu kwa wadau wake.
Aidha Dkt. Nsekela amefafanua kuwa Benki ya CRDB ilifikia wateja milioni 7.2 kupitia mtandao wa mpana zaidi wa huduma nchini Tanzani, Burundi, DR Congo, pamoja na Ofisi ya Uwakilishi ya Dubai, Pamoja na mageuzi ya mfumo yamesaidia kuongeza ufanisi katika mtandao wa utoaji huduma wa Benki.
"Benki ya CRDB inaongoza kwa mtandao wa matawi zaidi ya 261, ATM 732, CRDB Wakala 38,883 pamoja na vituo vya malipo na manunuzi 6,607, hatua iliyosaidia kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha nchini na katika masoko wanayo hudumia kitu ambacho tunazidi kujenga uzoefu bora kwa wateja kupitia teknolojia, huduma za kifedha jumuishi huku tukiendeleza dhamira yake ya kubadilisha maisha na kukuza maendeleo ya uchumi". Amesema Dkt. Nsekela.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRB, Prof. Neema Mori, ameeleza kuwa gawio hilo la shilingi 90 kwa kila hisa ni matokeo ya utendaji kazi imara wa Benki hiyo kwa mwaka 2025 na dhamira ya kuendelea kutoa thamani endelevu kwa wanahisa.
Prof. Mori, amefafanua kuwa Benki ya CRDB iliendelea kuonyesha ukuaji mkubwa wa kifedha mwaka 2025 ambapo faida baada ya kodi iliongezeka kwa asilimia 32.1 hadi kufikia Shilingi bilioni 728.6, mtaji wa wanahisa kufikia Shilingi trilioni 2.7 huku kiwango cha faida kwa mtajï wa wanahisa (ROAE) kikifikia asilimia 29.5.
"Mafanikio haya yameendelea kuongeza imani ya wawekezaji na kukuza thamani ya hisa ya Benki iliyofikia Shilingi 2,980 mwezi Aprili mwaka huu, Bodi itaendelea kusimamia ukuaji wa Benki kwa kuzingatia utawala bora, nidhamu ya kiutendaji, usimamizi madhubuti wa vihatarishi pamoja na uwekezaji katika ubunifu na teknolojia". Amesema Prof. Mori.
Aidha Prof. Mori Amewashukuru wanahisa, wateja, washirika, Menejimenti pamoja na wafanyakazi wa Benki ya CRDB kwa mchango wao mkubwa ulioendelea kuiwezesha Benki kufikia mafanikio hayo.
Kwa upande wake Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Frederick Nshekanabo amesema Benki hiyo imeendelea kuimarisha ufanisi wa kiutendaji na uwezo wake wa kuzalisha thamani endelevu kwa wanahisa kupitia usimamizi madhubuti wa gharama, ukuaji wa mapato na matumizi bora ya rasilimali.
Akiwasilisha taarifa ya fedha katika Mkutano Mkuu huo wa 31 wa Wanahisa, Nshekanabo, ameeleza kuwa uwiano wa gharama dhidi ya mapato yameendelea kushuka kutoka asilimia 45.7 mwaka 2024 hadi asilimia 41.6 mwaka 2025, hatua inayoonyesha ongezeko kubwa la ufanisi wa uendeshaji wa Benki hiyo.
"Matokeo haya yalienda sambamba na ukuaji mkubwa wa viashiria vingine vya kifedha, ikiwemo, Faida baada ya kodi kuongezeka kwa asilimia 32.1 hadi Shilingi bilioni 728.6, Mapato ya uendeshaji kuongezeka kwa asilimia 24 hadi Shilingi trilioni 1.88, Jumla ya mali kuongezeka kwa asilimia 33.6 hadi Shilingi trilioni 22.3, Amana za wateja kuongezeka kwa asilimia 36.6 hadi Shilingi trilioni 14.9, Mikopo imeongezeka kwa asilimia 32.5 hadi Shilingi trilioni 13.7 na Kiwango cha faida kwa mtaji wa wanahisa (ROAE) kuongezeka hadi asilimia 29.5". Amesema Nshekanabo.
Aidha Nshekanabo, alisema matokeo hayo yanaonyesha uimara wa msingi wa kifedha wa Benki ya CRDB, uwezo wake wa kuongeza thamani kwa wanahisa pamoja na nafasi yake kama taasisi kinara wa sekta ya fedha nchini na kikanda.
Akifumga Mkutano huo Mkuu wa 31 wa wanahisa wa Benki ya CRDB Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Dkt. Donald Mammari, amewashukuru wanahisa wote kwa ushiriki wao mkubwa na mchango wao katika kuendelea kuijenga Benki ya CRDB.
Aidha Dkt. Mammari ametoa pongezi maalum kwa Wanahisa vijana waliojitokeza kwa wingi kushiriki mkutano huo, akieleza kuwa ushiriki wao ni ishara ya imani, matumaini na mustakabali mzuri wa Benki ya CRDB.
Kaulimbiu ya Mkutano Mkuu wa Mwaka huu ilikuwa "Vijana na Uwekezaji katika Hisa".
Mkutano Mkuu ujao wa Wanahisa utafanyika siku ya Jumamosi, tarehe 15 Mei 2027, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha. (AICC).
Comments
Post a Comment