KIJAJI ATAKA TAARIFA ZA SENSA YA WANYAMA PORI KUTUMIKA KWA UMAKI ILI KUBORESHA USIMAMIZI WA HIFADHI NCHINI.
💢ATAKA TAASISI ZINAZO HUSIKA PAMOJA NA VIONGOZI WA SERIKALI KUSIMAMIA IPASAVYO KUTO ONGEZEKA SHUGHULI ZA KIBINADAMU NDANI YA HIFADHI.
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Ashatu Kijaji, amezindua rasmi matokeo ya Sensa ya Kitaifa ya Wanyamapori 2024/2025 na kusisitiza matumizi ya taarifa hizo kama nyenzo muhimu ya kisayansi katika kupanga na kuimarisha uhifadhi wa rasilimali za taifa.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo jijini Arusha, Kijaji alisema matokeo ya sensa hiyo yanaonesha hali halisi ya mabadiliko ya mifumo ya ikolojia nchini pamoja na athari zake kwa wanyamapori, akibainisha kuwa Serikali haina budi kuchukua hatua za kimkakati ili kulinda rasilimali hizo.
Alisema sensa hiyo imebaini mabadiliko makubwa katika baadhi ya maeneo ambayo hapo awali yalikuwa mapito ya wanyamapori lakini sasa yameingiliwa na shughuli za binadamu, hali inayotishia ustawi wa spishi mbalimbali.
“Ni lazima tutumie taarifa hizi kwa umakini mkubwa ili kuboresha usimamizi wa rasilimali zetu. Taarifa hizi zinatupa picha halisi ya wapi kuna changamoto na wapi hatua za haraka zinahitajika,” alisema Kijaji.
Aidha, alisisitiza kuwa sekta ya utalii inategemea moja kwa moja uhai wa wanyamapori, hivyo Serikali na wadau wote wanapaswa kuhakikisha rasilimali hizo zinalindwa kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.
Kijaji alisema Serikali itaongeza uwekezaji katika tafiti, ufuatiliaji na matumizi ya teknolojia za kisasa ili kudhibiti ujangili na kuhakikisha uhifadhi endelevu unafikiwa.
Aliongeza kuwa ushirikiano kati ya jamii zinazoishi karibu na hifadhi, watafiti na taasisi za Serikali ni muhimu katika kufanikisha malengo ya uhifadhi wa muda mrefu.
Katika hatua nyingine alisema matokeo ya Sensa ya Wanyamapori 2024/2025 yanaonesha mafanikio makubwa katika juhudi za uhifadhi, ambapo idadi ya wanyamapori imeongezeka kwa ujumla ikilinganishwa na sensa ya mwaka 2014 huku baadhi wakupungua kwa kasi kubwa.
Alisema sensa hiyo iliyofanyika kati ya mwaka 2024 na 2025 ilihusisha maeneo yote muhimu ya ikolojia yakiwemo hifadhi za taifa, mapori ya akiba, misitu, shoroba za wanyamapori na maeneo mengine ya uhifadhi.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, kati ya aina 19 za wanyamapori zilizofanyiwa tathmini, aina saba zimeongezeka kwa kiwango kikubwa, 11 zimeendelea kuimarika, na aina moja pekee ndiyo imeonesha kupungua—hali inayohitaji hatua za haraka za uhifadhi.
“Hii ni nyenzo muhimu kwa Serikali na wadau wote katika kupanga mikakati ya matumizi endelevu ya rasilimali za wanyamapori na kuendeleza sekta ya utalii,” alisema.
Amezitaja taasisi zilizoshiriki zoezi hilo kuwa ni pamoja na TAWA, TANAPA, NCAA, TFS na TAWIRI, akizipongeza kwa ushirikiano wao mkubwa uliofanikisha zoezi hilo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maliasili na Utalii, Timothy Mzava, ameitaka Serikali kuanzisha mjadala mpana wa kitaifa kuhusu mustakabali wa Tanzania kutokana na ongezeko kubwa la watu.
Akizungumza katika uzinduzi wa sensa hiyo, Mzava alisema kasi ya ongezeko la watu inapaswa kwenda sambamba na mipango madhubuti ya maendeleo na uhifadhi wa rasilimali za taifa
Alisema takwimu zinaonesha Tanzania ilikuwa na takribani watu milioni 34 mwaka 2002, huku sensa ya 2024 ikionesha zaidi ya milioni 61, hali inayoashiria ongezeko kubwa la mahitaji ya ardhi na rasilimali.
“Ni lazima tuwe na mjadala wa kina kuhusu Tanzania ya miongo ijayo. Bila kufanya hivyo tunaweza kukabiliana na changamoto kubwa zaidi,” alisema Mzava.
Alisisitiza kuwa sekta za maliasili na utalii zitaathiriwa zaidi, hivyo mikakati ya muda mrefu inahitajika ili kuhakikisha maendeleo na uhifadhi vinaenda sambamba
Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Toba Nguvila, amesema matokeo ya sensa ya wanyamapori yatasaidia kuboresha mipango ya uhifadhi na kukuza sekta ya utalii nchini.
Alisema Arusha, ikiwa kitovu cha utalii, inathamini juhudi za Serikali katika kuhakikisha takwimu sahihi zinapatikana kwa ajili ya maamuzi ya kisera na kiutendaji.
“Matokeo haya yanatupa picha halisi ya rasilimali zetu. Takwimu hizi zitasaidia kuimarisha uhifadhi na kuhakikisha sekta ya utalii inanufaisha kizazi cha sasa na kijacho,” alisema.
Nguvila aliongeza kuwa Mkoa wa Arusha utaendelea kuboresha mazingira rafiki ya uwekezaji na utalii kwa kuhakikisha amani na usalama vinaendelea kudumishwa.
Aidha, alitaja mipango ya mkoa kuandaa mkakati maalumu wa maendeleo ya utalii wa miaka mitatu utakaolenga kuongeza ushindani wa Arusha kimataifa.














Comments
Post a Comment